Friday, 9 November 2012

Somo - Khalati/ Shangazi kwa Mtoto wa Kike Aliyevunja Ungo....


Amira Msallem

Somo   Kiswahili huwa ni khalati/shangazi wa mtoto wa kike.  Mtoto wa kike anapofika miaka kumi na nne au tano hivi huvunda ungo. 

Kuvunda ungo ni kubaleikh au kupata hedhi kwa mara ya kwanza.   Kunao uwezakano kwa mtoto wa kike kuvunda ungo mapema kuanzia miaka tisa na vile vile kuna wale huchelewa.  Haya yote hutegemea:
·         Kizazi ya familia
·         Mazingara yaweza kusababisha kupata hedhi mapema ama kuchelewa kwa mtoto wa kike.
·         Vyakula huchangia pakubwa pia

Yote tisa, kumi kuvunda ungo kwa mtoto wakike na furaha kubwa sana khaswa khaswa kwa mama mzazi.  Kwani mtoto wa kike anapo baleikhe ama kuvunda ungo, huwa ni ishara nzuri:
·         Yaonesha kuwa amekamilika kuwa mwanamke
·         Amevuka daraja na kupanda cheo kwani sasa ana julikana kama Mwari/Mwanamwali
·         Ni ishara kuwa sasa anaweza kutafutiwa mchumba, amekamilika kuwa mke nyumbani.

Pindi tu, anapovunda ungo mtoto wa kike mara ya kwanza, mtoto yule hupelekwa kwa khalati/Shangazi yake ama ukipenda (SOMO) kupata elimu muhimu  ya;
·         Dini
·         Mila na desturi
·         Usafi wa mwili wake na nguo zake


DINI:
Dini ni muhimu sana na pia nimuongozo bora.  Mtoto wa kiislamu akiinukia tayari hufundishwa dini  ama hukuwa na dini lakini hata hivyo pindi mtoto wa kike anapo baleikh ama kuvunda ungo somo humfundisha tena kuhusu dini na hedhi kwa urefu na kwa njia njia yakufahamika .  Khaswa mambo ya muhimu na lazima kwa mtoto wa kike kama:
·         Umuhimu ya hijabu kwa mtoto wa kike
·         Mavazi ya sitara na heshima
·         Sheria ya dini unapokuwa  kwa hedhi na namna yakujitwahirisha
·         Mwari au mwanamali haruhusiwi kukurubiana na mtoto wa kiume
·         Usafi na umuhimu yake kwa mwanamwali wa kiislamu.

MILA NA DESTURI:
Mbali na dini mila na desturi ni muhimu kwa mtoto wa kike, kwa sababu baada ya kubaleikh huwa kuna uwezakano ya kuolewa kwa haraka kama desturi ilivyo bila ya kupoteza wakati, naiwapo mwari/mwanamwali atakuwa hajui mila na desturi huwa ni aibu kubwa kwa wazee wake na familia.

Somo yake mtoto huchukuwa jukumu  nakuakikisha kwamba Yule mwanamali ana jua mila na desturi.  Mtoto yule wa kike atafundishwa na somo :
·         Kuingia jikoni afundishwe kupika kwa ustadi  na namna ya kuandaa mankuli.
·         Heshima na adabu njema kwa wazee, wanaomshinda kwa umri
·         Mtoto wa kike hafai kucheka kwa sauti ya juu ama kuzungumza
·         Mtoto wa kike hufundishwa kuwa na haya na khaswa anapozungumza na watu wazima wake ni sharti  azungumze kwa sauti ya chini na unyenyekevu na adabu
·         Mtoto wa kike anapo baleikh hufundishwa kujisitiri na kuwa mustarabu, anapoketi chini panapo watu wazima akae kwa heshima, anapolala, atakiwa kulala kitumbo tumbo
·         Avae mavazi ya sitara na heshima
·         Awe ni maridadi wa mwili wake, umaridadi wa usafi na umaridadi wa akili na kuwa na busara.

Haya yote niliotaja ni baadhi tuu, ya mafundisho na matayarisho kwa mtoto wa kike anapo baleikh au anapo vunda ungo .

MTOTO WA KIKE ANAPOVUNDA UNGO MARA YAKWANZA AU ANAPO BALEIKH
Mtoto wa kike anapovunda ungo mara ya kwanza au kubalekh  hupelekwa kwa shangazi/khalati (SOMO) kwa mda ya wiki mbili kuelimishwa elimu mbali mbali yanayopasa mwanamke kujua , kisha mwari Yule huregeshwa nyumbani kwa mamake mzazi akiwa na elimu yakutosha kumsitiri , akili huwa ya kiutu uzima, huwa amebadilika kwa tabia na ujihisi amepanda daraja au cheo nyingine katika maishani mwake.

Mwanamwali Yule huregeshwa kwa somo pindi tuu akiingia kwenye hedhi tena kwa mara ya pili, lakini tofauti na awali ama mara ya kwanza  safari hii ya pili huwa ni kama mtihani. Somo ataka kuangalia jee aliyofunzwa mwari alishika? Au amefaulu ? lau atakuwa ameshika aliyefunzwa na somo wake basi akimaliza hedhi yake mwari huregeshwa nyumbani kwa kwao na zawadi ya leso gora mbili, mmoja huvaa na nyingine akakibeba.

Baada ya hapa somo hana kazi tena mpaka siku ya kuolewa mwari wake.SOMO – KHALATI/SHANGAZI
KWA MTOTO WA KIKE ALIYE VUNDA UNGO AU KUBLEIKH
WA KISWAHILI
NA
AMIRA MSALLEM
 

No comments:

Post a Comment