Monday 5 May 2014

NGOMA ZA KIPOKOMO



 
MAJ. RTD SWALEH ODHA
CELLPHONE NO: 0721 308 594
Email: odhaswaleh@yahoo.com
P.o. Box 87440-080100
Kiembeni Estate – Mombasa










UTANGULIZI:
Mila ni kiungo muhimu katika maisha ya mwanadamu. Kwenye kunga ya maendeleo, mila ilipachikwa miongoni mwa elimu, dini, afya, ulinzi, ukulima na mazingira; yote yakiwa chini ya mwamvuli wa nguzo ya kijamii, mbali na kiuchumi na kisiasa. Kati ya viungo vyote hivyo mila, ndiye uti wa mgongo na kidhibiti mwendo cha jamii duniani. Hivi kwamba jamii ilipaswa kuendeleza sera yake kijamii kwanza ndipo itambulike kiuchumi na kisisa. Mfano ni Uchina, ilipata jina kisisa baada ya kumiliki barabara ukulima. Japan na teknolojia viwandani kwenye sera za kushindana kukuza vipawa viliwafanya wenyeji kuwa matajiri kiuchumi. Milki za Uingereza na sera zao za utawala wa dunia ni mfano tosha wa kijamii. Marekani haikubaki nyuma kwani kila mielekeo yao ya muungano wan chi hamsini ziliipa nguvu nchi nzima kwa ujuzi tofauti tofauti. Kama mzungu alizunguka kutalii ili aendeleze utafiti wake , naye mwarabu vile vile aliishi kwingi kuzabuni ili biashara yake inoge; biashara ni kitengo cha uchumi lakini tabia yake si siasa bali ni kunga ya kijamii. Kwa jumla, mtu kuendelea kwa vyovyote vile ni sharti mila. Na hivyo basi bila ya mila, pana ila. Ndiposa kauli ya ,’Mwacha mila ni mtumwa’’ ikaja. Mtu mathalani hakupiga kura kuzaliwa

alipozaliwa. Na pindi ukizaliwa Mpokomo huna tena hiari ya kuchagua eti ugeuke na uwe Mkamba. Upende au usipende huna budi, utabaki kula, kuvaa, kufurahi, na kuhuzunika.

NYIMBO BILA NGOMA:
Mpokomo pia yuko na mila zake. Aliimba na kucheza. Aliimba nyimbo za furaha na za huzuni pia, kwa sababu nyingi tofauti tofauti. Kwa mfano, Mpokomo aliiimba Gassa/Kittoko bila ya ala yoyote ile ya muziki, Aliimba bila ya kucheza na akiwa chini kitako au kalala chali, hakusimama wima. Alikiimba kittoko hicho aidha kutahadharisha kwa mfano (Jihadharini-Mende), Kejeli kwa mfano (Ningali Kijana-Mende), Mapenzi kwa mfano (Together- Dr. Niko)na Hamasa kwa mfano (Wanawake wa Ndera- Ise Viera). Nyimbo za aina hii huimbwa wakati wowote hasa usiku. Na washiriki ni waume akiwepo mwana dada fulani pengine bibi wa mmoja kati ya waimbaji tena mraibu wa nyimbo kama hizo. Hapa ni furaha tupu. Kwani nyingi wa nyimbo hizo ni tumbuizo sana mume kumuimba mwanamke akimsifu, akimsibu na kmuumbua watu wasikie urembo au ila yake muumbuliwa huyo pasina mwenyewe kuwepo.

Kkosa ya Dani ni mchezo wa watoto wa kipokomo ambapo ngoma haikutumika. Michezo mingine ni watoto wa kike mingine ya kiume na mingine iliwajumuisha wote. Mfano :
Majjilingao-Mchezo wa watoto wanaposhikana makundi mawili wakipishana, wanapita kwa watoto wawili walioshikana mikono wakiweka mtego wa kunasia   huku wanaimba usiku;  -Haijjafiiko? He! He! e!  -Majjilingao ho ho lingo, majjilingao kittattafule.  -Ngao ya mabombwe, fumo ddyakuttora.





Mpesi-Mchezo wa watoto wanapoketi chini na kufanya dori, miguuni pana kitambaa kinazungushwa huku na huko kushoto kulia na nguo imefunika gubi gubi mwanzo wa kiuno kukiimbwa usiku;   -Mpesie, mpesi karitto, ikiya wenye bbabbaa.
Kode-Mchezo wa watoto wa kike wakichimba kishimo ardhini na kuweka mawe. Hurusha moja juu huku wakitoa na kusukuma zingine ndani kulingana na hesabu ya anayecheza bila ya kuimba.Mchezo ni wa mchana.
Tteba-Mchezo wa watoto hasa wa kike wakichora miraba ardhini kiasi cha wachezaji. Kipande cha mawe hutupwa kinyumenyume na kikiangukia chini ni,’tteba’, mchezo huanza kwa kurukaruka kutumia mguu mmoja mchana.
Pofu-Pafle-Mchezo wa watoto wakifukuzana majini aidha mtoni au ziwani. Ni wimbo alafu mbio wakipiga mbizi,mbio na kachombe kwa wimbo na kushangilia hasa nyakati za mchana;  -Pofuo-Pafle, Ddya mama- Ee, Aniaggiye-Ee,Ddyakwe!
Kinu Kya Hawito-Mchezo wa watoto nyakati za usiku wanapojilaza kwa amri ya mmoja wao, Ngalingaliee!; Wanalala macho juu, wakinyoosha mwili mzima:   - Kinuo kinu kya Hawito,kya mchelechele bbwoya bbwoya. –Mwezie-ee! Ee!,mwana chingicha mwana e mwana chingicha.   -Chiko chikoo! Haya.
Fiche (Rare)-  Mchezo wa watoto kufumba mkono nyuma migongoni na kuwambia wenzi wao watambue walichoficha kuwa kikulia au kushoto.                                                                                                                               
Chio-Mchezo wa watoto usiku wakifukuzana kwa zamu huku mmoja kafungwa kitambaa cha macho asione na kwa nyimbo;- Amfu kattuttu- ttuttuya, Nije ne fumo nije ne ttora? Njo ne fumo. - Chio kafwe macho, chio kaona.Huyo mhangaisheni huyo.
Msupepe-Mchezo wa watoto wa kupesapesa miguu hasa wanawake wakichuchumaa wawili wawili huku wamegeukiana wakiimba na kupigapiga mchanga kwa mikono yao yote;  - Msupepe mchanga moto kwauona.


Kinamddabbe-Mchezo wa watoto wakikimbizana ndani ya maji, nje na kwenye nyumba inayojengwa, hasa nyumba ya miti miti.Mmoja anafuata mwingine amguse huku wakiimba;
- Kinamddabbe, unakyo-anakyo.Mbio…..!
Akosee- Mchezo wa watoto mchana kwenye dori hasa wanawake. Wanapokezana viguguta  wakiimba;- Akosee nyaa zipho hamkuna mongo wa nyama. - Hoo hohoo Maramba kachi mwayano maramba. - Mamo niphe yukombe nikadye marikka nyamo.  - Kkosao mfunyeni kakosa.
Tandaule-Mchezo wa watoto wakinyoosha miguu wakikaguliwa kwa nyimbo;-
-Mosia tandaule nyota kwa mlima katiti simbanyo naiya kwa ngombe bburanyinga ho!.Ngombe zenu bburungale kwa jili kwa ngombe. Mwananimbwa bbwa, maddindye ho, mwananimbwa bbwa!      
-Moja na moja tandaule kwa magguyu ggwanya ggwanya, madindye hoo mwana nimbwa bbwa bbwa bbwa!
                                                                                                                                                     
-Koko kokoya na malugga sangarse mumina. Mumino washindi shindi kajja waddoddo rubbesa. Abbo, kalimaddo, manguddo, ttalabba.
                                                                                                          

-Bbocha karara, magguyu chingicha, maneno mabaya, ttumbaku na nusu, nusura fwe!
                                                                                                                                                                       
 
-Dangulo dangulo, he ntanta yuwa, he yuwa yuwa mai, he mai mai kulotta, he kulotta kulotta simba, he simba  simbaegguru, he gguru gguru kongwe, whende kwa vironda.
Kwa nyingi nyingi- Watoto bado wakiwa kitako na miguu yao wameinyosha. Mwenye kuhisabu na aliye kiongozi anapitisha mkono na kuitingisha kofia ya goti.                                                                                                                                 
 
-
Kwa nyingi nyingi kwa nyingi nyingi,kona unazimbika seggera unga, kuko kumbika kumbuka kwa nyingi nyingi. - Nkuruttume nyade, saanga nyade.  - Ggumbu ggumbu ggumbu sole!

Dangalola-Huu ni mchezo kama kinamddabbe, watoto hufukuzana kwenye uwanja bila ya kwenda mbali. -Daanga loola-Samakia. Daanga loola- Samakia. Hasina nampata- kwampata. Hasina nampata-kwampata.
Addirise kiguyu-Mchezo wa watoto usiku wakishikana kwa pamoja na kurukaruka kwa mguu mmoja huku wakiimba;- Addirise kigguyuo e nangere, addirise kigguyu ajjeanisehe nangere. - Mwanahajjuyu ggoneyea keso maggura haonana.
Mwaraggidde- Mchezo wa watoto wakiwa chini kitako. Makundi mawili wamefuatana kwa mlolongo na kiongozi wao akimlenga kwa bunda la nguo amchukue kila anayempiga.Wengine wakijificha nyuma ya mgongo, huku wanaimba; - Mwaraggidde- buu, mare hekaani-hekaani
Piropiro-Mchezo wa watoto:  -Piropiro chamara, asiduna nayawe.   -Ggoromicho ee! Micho, koonde na konde
Kwangure mongo- Mchezo wa karibu kumalizia michezo wakati wa usiku watoto wanasinzia ishara ya, ‘twende tukalale.’ Mistari ni miwili na kila kalabba watu wawili hutawanyika na kutoka mistari yao upande upande na kwenda kwao;
- Kwangure mongo, haya. Mwanangu kalabba kalabba, haya.
- Mwanahajjuyu ggoneyea keso maggura haonana.

Ngware ni nyimbo za Kipokomo za dini kwa ndugu wakristo hasa wa chini- (Milanchini) Tana Delta. Huimbwa pia bila ya ngoma. Na sana, ni katika kusherehekea siku kuu ya Krismasi na mwaka mpya. Huimbwa usiku wa kuamkia tarehe moja Januari na washiriki ni wake kwa waume. Mfano wa nyimbo ni (Nilekeze Pwani) na (Naikurubia).
Mattalili huimbwa bila ya ngoma na ndugu waislamu wakati wa kuomboleza mtu akiaga na kabla ya kuzikwa. Wanawake huizunguka maiti ikiwa kitandani na hata wakiwa nje ya nyumba huku wakilia. Pindi mtu akifa iwe usiku hadi mchana mpaka azikwe, basi ni nyimbo tu za  huzuni.
Himatta ni nyimbo mashambani wanawake au waume wanapokutana kwa kulimiana. Ni jembe nyimbo. Mfano (Kirura Ami Saduna Kirura).
Funya ni nyimbo isiyo na ngoma kwa akina mama wapokomo. Mtu akiasi au kuwakosea wanawake, aidha sheria zao kuvunjwa hasa na waume, wanawake hujumuika kwa kumlipiza kisasi kwa kumkwangura kwa makucha au koa za mtoni. Humwimbia nyimbo za kumuapiza na kumlaani huku wakilia kwa mfano (Whendeni wake whendeni) na (Kahuddawia).

Yavia  ni hali ya kumtoa kipusa na kumkubali katika hali ya umama. Kwamba sasa ametosha kulea mume na nyumba yenye watoto. Kwamba akubali pia kujihusisha na hali ya maisha kwamba aliyekuoa amekuchongea. Nyimbo zake ni;( Unauke kauyawa kafungwa polwe ddya kichwa).
Sosobha ni kibembeleza mwana. Mtoto anapolia aidha kulia kwa kumkosa mama mzazi, kulilia njaa au maumivu, mkubwa wake humbembeleza. Ni kutokana na nyimbo ya aina hii ambapo nchi ya Kenya imejipatia wimbo wa taifa. Mfano wa nyimbo hizo ni:
Woi woi mwano, wanyoko waime, waime mupunga, mupunga nde wako, nde wako we kuddya, we kuddya unyamaiye njayoo!!( Oi! Mtoto nyamaza, ili wazazi walime, ili walime mpunga, wewe unapenda sana kula mpunga,ukila tu, huwa unatosheka).

Mwana nyamaya mwana nyamayo, nyoko kenda pwanie, sowe kenda pwanie! Na kuninyea na kunikojeeo.(Wee mtoto nyamaza, mamako alienda mtoni, babako alienda mtoni, wewe unanikunyia na kunikojelea).
Mddondo mddondo, hayuno mwana kaiyaani njoo muuddye. Mddondo ywangu kichwa na mukia.(Mdudu mdudu tafadhali, huyu hapa mtoto analia fika umtafune. Mdudu muhibu mwenye kichwa na mkia).
Bee mddondo be! Bee mddondo be! Akuddobbee ni naani, whende hukawabbigge wantu wa makondeni mwezi uyawa ni naani? (Ee mdudu! Ee mdudu! Nani alokuchokoza, tuende tukawapige wantu wa mashambani. Mbalamwezi ulitoka, ni nani?).
Akiiyoiyo humudoma mikomani, naye kanamba nicheze. Kajjende mwana, kajjende mwana naye njwa kiiyoiyo. Woi woiyee! Nyamaya kimye. Siiye mwano, siiye mwana nunu, nyamaya kimi. Nyamayo, nyamaya mwana bee! Nyamayo, nyamaya mwana bee kisasuzi. Kisasuzi mwana jjongoyoyo bee! (Analia na tumemuokota kichakani, na ananiambia nimuimbiye. Mtoto hanyamazi, na katu hatulii bado analia. Lo! Mungu wangu. Mtoto anyamaze. Usililie tena, usilie mtoto mzuri. Nyamaza kimya. Nyamaza kasha utulie tuli. Na ukitulia nitakufurahisha na nikupe kitu kizuri).
Hayudde nkimo, hayudde nkima, hayudde nkimaa mkoshoro karebbani kyambo (Ndiye Yule tumbiri, tumbiri mgiryama anasubiri chambo).
Nyalilo ni mchezo wa watoto. Koko ya embe ilitobolewa na kuwekwa kamba katikati. Inazungushwa koko hiyo na pindi ikivutwa huleta kasi fulani  na mlio tosha kuitwa mchezo.
Mpheru ni mchezo wa watoto wa kupiga pia ya mti. Mti huchongwa kiasi na hutegemea aina ya mti. Kibati kilichofungwa na mti kwa kamba hutumika kama usukani wa kuendesha pia hiyo. Kila kinapotandikwa huvuma na kuleta mlio. Watoto wawili au zaidi huvigonganisha vizuu hivyo na kinachozunguka na kizito kilichochongwa kwa usawa huviangusha vingine dhaifu.
Mphujju ni mchezo karibu sawa na mpheru wa kuzungusha pia. Tofauti ni kwamba, mpheru ni kigongo cha mti wowote, huchongwa. Mphujju, ni mmea au mti maalumu unaoitwa m’mphujju. Mti huo huzaa matunda aina ya mapera nayo huitwa mphujju. Tunda hilo likikauka mbegu zake humwagika tunda likitobolewa katikati. Ni kama mpira uutoboe juu na chini sawa sawa. Kijiti huchukuwa nafasi ya matundu yale mawili. Kwa kutumia kijiti kilichojikunja cha upongoo kutoka kwa mkindu, kamba hufungwa na ikizungushwa kwa kijiti cha tunda hili na kuachiliwa, tunda hucheza ngoma nzuri sana hadi mwisho hupumzika. Ni mchezaji airudie kazi hiyo tena na tena.
Ggao au saddyekka ni mchezo wa wazee wa kiume wakijitumbuiza barazani. Huu ni mchezo wa bao na unachezwa katika jamii nyingi duniani. Hauna wimbo ispokuwa kufanyiana mizaha kama vile kwenye karata, keramu  na drafu.


NYIMBO NA NGOMA:
Ngwili ni nyimbo za ngoma kwa wanawake wa kipokomo mwanamke akizaa. Ngoma hii ala yake ni debe tupu lenye kuleta makelele ili anayezaa asisikike sauti akilia kwa maumivu hasa, anafichwa mtu mume asiijue siri ya uzazi unaumpata mkewe. Sauti ya hamasa na kushajiisha wanawake wakutane kwa haraka ya, Yee Wake! Kisha nyimbo mfululizo pamoja na msukumo wa anayezaa, huku wakimpiga na kumchuna. E kavyayo, ee kavyayo! Yaani, o! amejifungua. Huimbwa wakati wowote, usiku au mchana.
Beni huimbwa sana na wanawake wa Kipokomo kwa ndugu wakristo. Ni ngozi iliyowambwa kwa pipa kubwa litoe mlio mzito na watu warindime kama ilivyo ngoma hiyo.






Samai
ni ngoma ya kidini iliyoibuka katika tamasha za kuadhimisha siku ya kuzaliwa mtume Muhammad. Ni gwaride la sarakasi katika kuendeleza maghani ya maulidi barzanji na maulidi ya Kiswahili. Siku hizi, Samai imemea miguu na kuwa Zamuni, yaani kwata. Kama kawaida vazi la kanzu na kofia huvaliwa na vijana wakijumuika kando na wasichana wenye buibui. Ala za muziki ni ttwari, kigoma na zumari. Kwakuwa Mpokomo mwingi ni muislamu na amepakana na Mswahili, dini imekuwa ni mila yake na tamaduni ya uislamu katika kuijenga elimu ya dini na dunia alitumia ushairi, midundo na mahadhi ya kiislamu. Bila ya shaka hatuna budi kuingiza mada hii katika kundi hili la ngoma hasa ikikumbukwa ya kwamba ttwari  pia hutumia ngozi kama vile ngoma. Katika fani hii, hata kama si mwanzilishi, Mpokomo amebobea na kukubuhu ujuzi mwingi wa ngoma hii zaidi kuliko kabila yoyote Pwani.
Mtu huzaliwa na akawa mtu mkubwa. Akiwa njiani mtu hupitia mambo kadha wa kadha kimaisha ili akubalike katika hadhi, tabaka na daraja aliyonayo. Kwa mfano kijana hutahiriwa ili astiri uume wake huduma bora kwa mkewe.  Kijana anapotahiriwa hupitia daraja tofauti tofauti kule jandoni. Tohara (Ntinye) ni wakati wanapofanyiwa kitendo na ambapo ni mwanzo wa ngoma, alafu Tohara (Riggi) wakati kijana ashatahiriwa na mwisho ni Tohara (Lwebbe) kijana yuko tayari. Zipo nyimbo na ngoma zake hapa: (Yarhigha na Mbele), (Lele Mwobbe) na (Usikile Ubbaratte).  Miri ndiyo ngoma inayochezwa mchana kutwa na usiku kucha. Hujumuika wake kwa waume ili kuwangojea vijana watoke jandoni na kuelekea makwao. Njuga za kutengenezwa na miyaa huundwa na kuvaliwa miguuni kwa waume. Nkanyiki, shanga, ngorosho na kkone, huvaliwa maungoni, kiunonu na shingoni. Mikononi wameshikilia nchoncho huku wamevalia ttama vichwani mwao.  Wanawake nao ni Vumba vichwani mwao, vichida shingoni, Hida maungoni pamoja na shanga. Nyimbo za mchezo wa Miri ni nyingi, bali sana ni (Jjabha Kayulelo)


Gganga ni aina ya ngoma ya Kipokomo ichezwayo na wazee wakienda kurogga, wakitoa
huduma ya matibabu kutoa jinni  (Kidumbwe)na kufurahikia. Kwa mfano wanaimba: (Gganga mekuya). Hapa ni furaha na mchanganyiko wa huzuni kwa wote. Gganga na Miri ni viungo tosha kwenye halmashauri ya serikali kuu ya wazee wa Kipomomo zama zile, yaani Kijjo na Waggangana. Washingo huchezwa na watu wa kawaida kufurahikia jambo au tukio Fulani.

Wanawake kwa waume wenye rika moja ndio washiriki. Usiku au mchana ndio ngoma hunoga. Mfano wa nyimbo yake ni: (Muharia Ywangu).


Kittoko ni mchezo pia huchezwa wake kwa waume sana kwa kufurahikia hali Fulani wakati maalumu kama vile baada ya kazi, mavuno na arusini. Nyimbo kama (Mattolibi walonioza).

Ngoma hizi zote hapo juu hutumia ala aina ya ngoma kubwa, ikiandamwa na kijigoma kidogo na kijidebe kilichogongwa na vijiti. Pembe au koa hupulizwa kuletwa shangwe na vigelegele.
Mwaribe  huchezwa kwa ajili ya furaha vile vile usiku au mchana. Ngoma aina ya sondo na pia pilingwa, vumi na uttasha ugongwao na vijiti hutumika. Mfano wa nyimbo iimbwayo wakati huo ni: (Mboya si ddya kuhenda).

 Ttaireni ni ngoma ya mzuka au kutoa mapepo yaliyowakabili wagonjwa. Nyimbo aina hii ndizo huimbwa: (Farasi Wangu Panda). Mgonjwa anaweza kuwa mke au mume. Utasha, Vumi na kijigoma ndizo hutumika.
Wanawake wakijifungua (Ngia Nyumbani), hukaa ndani ya nyumba kwa siku thelathini na tisa bila ya kutoka nje. Siku ya arubaini ni sherehe ya kutoka (Yawa Nyumbani). Mchezo huu ni wa wanawake, tena wale waliopata bahati ya kuzaa hata kama mtu amezaa kisha mtoto akafa hajazaa tena. Mfano wa nyimbo zao ni (Hida Kiwaluwalu). Kidundu (Kikaha) ndicho kinachotumika kama ala ya kuchezea ngoma. Ngoma ya aina hii ambayo kwa jumla ni ngoma ya akina mama pekee, huitwa (Mea Wake). Bali watu wa jamii ya juu huita  Kingika (Wantua dzuu) na Kuphanga (Milanchini).

AINA YA NGOMA:
Wapokomo wako na ngoma nyingi nadhani kuliko kabila yeyote nchini Kenya.  Ngoma hizi nyingi ni za kuwambwa na ngozi aidha ya mnyama mwitu kama nyati, kuro, swara au mnyama wa kufugwa kama mbhzi na ng’ombe. Mti maalumu kulingana na itikadi huchongwa kwa namna Fulani ili kukidhi haja ya mchezo ule. Wakati  mwingine chuma hutumika endapo mti ulikosekana kuchongwa kwani si kila mtu huchonga. Vipo vifaa vingine vingi vinavyotumika kuunda ngoma. Vifaa vingine ni siri ya wazee wa Gassa. Hivi ndivyo vifaa vingine: Ngoma mzuka, ngoma ttaireni, ngoma wggangana, mwaribe, pilingwa, vumi, ttwari, beni, uttasha na kadhalika.


Story Prepared  By
Fatma Mansoor
Elimu Asilia , 2014
Research Institute of Swahili Studies in Eastern Africa (RISSEA)
National Museums of Kenya