Tuesday 20 August 2013

Ngoma za Kitamaduni, Malindi.......


UTANGULIZI

TAREHE FUPI YA MUANDISHI

Abud Salim Mbarak Bazmaleh,
Mimi nilizaliwa kati ya 1944 na 1945 katika mtaa wa Kwajiwa – Malindi. Katika khati ya kuzaliwa imeandikwa tarehe 15th September 1946. Tarehe hii iiandikwa kwa munasaba wa kuniwezesha mimi kutukuwa mtihani wa KAPE (Kenya Asian Primary Examination). Kwa wakati ule ukiopita umri wa miaka 14 huendi shule ya upili, kwa hivyo marehemu Babangu (Mungu amuweke Pema – Peponi) wakati akiandikisha hati ya kuzaliwa 1953 yeye na msaada wa msajili wakati ule wakaamua hivyo.

Nilipata ajali ya kuunguwa tumboni katika mwezi wa Ramadahni siku moja kabla ya Idd Al Fitri baina ya 1948 na 1949. Mimi sifahamu na wazee pia walisahau hawakujuwa ni mwaka gani. Daktari wakati ule alikuwa Dr. Rozenger, yeye alimshauri marehemu Babangu kunipeleka hospitali ya Makadara Mombasa.  Sipitali ya Makadara ilikuweko ambako sasa ni jingo la Posta Kubwa Mombasa, Salim Road, (sasa ni Digo Road)
Mombasa nilikaa Mwebe wa Tanganyika na ni kishughulikiwa na marehemu mjomba wangu na shangazi yangu (Mola awarehemu wote na kuwaweka mahali Pema peponi) Mwisho wa mwaka wa 1951 nilirudi Malindi na Jan. 1952 ni kaingia shule ya Sir Ali bin Salim, nikianzia Qur’aan class.
Jan 1953 nikaanza Std. 1 ni  kaendelea vizuri hadi std 7 mwaka wa 1960 mwezi wa November, ni kachukuwa mtihani wa KAPE na Al- Hamdulilah nikapasi kwa “Grade III”.
Jan 1961 nikaanza shule ya upili ya Arab Secondary  (sasa Khamisi Secondary School) kama “Boarder” mwanafunzi wa kulala shule. March 1964 nikiwa form 4 nikaacha shule kwa sababu zisioepukika. Mwezi ule nikapata kazi katika idara ya “Government Coast Agency” kitengo katika Ministry of works.
Mimi nilikuwa ni kicheza wa mpira wa miguu, mkimbiaji wa 220yrd na 400yrd wakati ule (sasa ni 200mt na 400 mts) na Hokey.
Nilijiuzulu kutoka kazi ya serekali mwaka wa 1970. Baada ya hapo nikafanya kazi tafauti tafauti zilio nipeleka Bungoma, Kisumu, Mbale Uganda na nikamalizia Saud Arabia. Saud Arabia nilienda mwaka wa 1980 mwezi wa 3 na nilifanya kazi kwa miaka 14.
Niliporudi Malindi ni Kafunguwa offisi ya udalali na nikapata liseni ni kafanya kazi kwa miaka 3. Baada ya kuja mipango ya sheria mpya nikakosa liseni kwa kiwango cha elimu walicho hitaji.

Nikafanya kazi kama “Part time Accountant” kwa matajiri Fulani kwa vile nilikuwa na Diploma ya “Book keeping” wakati ule ni kajishughulisha na Kazi za kijamii kwa upande wa serekali na Mashirika yahaki za binadamu. Nilikuwa Treasurer wa Malindi Constituency Aids kwa miaka 10.  Wakati huo pia nilikuwa katika Education Board kwa miaka 10 na pia Barani Secondary School Board of Governors kwa miaka kumi.
Nilikuwa secretary wa SUPKEM na pia Monitor wa FIDA “Chama kinachosimamia na kutetea hakia za wanawake na watoto” Nikatuzwa Special Category Human Rights Award 2006.

Hata hivi ninashughulika na kazi za kijamii kama mzee wa mtaa wa Kwajiwa na Secretary wa Malindi Council of Swahili Elders.
Hii ndio tarehe yangu kwa ufupi sana kwani hapa sipo pahali pakuleta tarehee yangu bali nilitaka alioandika kumbu kumbu hii ajulikane alikuwa ni mtu gani na waina gani. Pengine unaweza kupata maelezo mengine kupitia Google “BAZMALEH” ambapo ukifika katika jina langu unaweza kupata maelezo zaidi.

Unaweza kuwasiliana nami kupitia 
P. O. Box 152, 80200, 
MALINDI, KENYA 
Email – abubazmaleh@yahoo.com
Mobile No. +254 724 336 113.


LUGHA NILIO CHAGUWA
Tangu nilipokuwa shuleni nilikuwa nikipenda kuandika makala ya Kiswahili na takriban mabuki yangu yote ya shule nilikuwa nikiandika ushairi katika karatasi ya mwisho ya daftari langu.  Jambo ambalo lilikuwa likinipa shida ya kupata daftari jipya kutoka kwa mwalimu likimalizika.
Pia nimeandika vitabu kadha ambazo sikufaulu kuchapisha za ushairi na hadithi za kutunga. Kwa vile napenda kuandika Kiswahili kwa ajili ya kuituza ndio nikaamuwa kuwa hii kumbukumbu niandike kwa lugha ya Kiswahili – lugha ninayo ipenda na hujinaki nayo na kuienzi.
SHEREHE
Malindi ilikuwa si mji mkubwa uliokuwa na wakaaji wengi wakati ule. Pengine kama elfu 50 hadi 75 watu wenyewe walikuwa wa kijuwana. Sehemu nying ya mji wa Malindi ilikuwa ni matuka ya nyasi na miti ya mibaraka kwa wingi katika sehemu nyingi pamoja na mikunazi, wakaaji wengi walikuwa ni Warabu Wahindi, Waswahili na Wagunya (Wabajuni). Wamijikenda walikuwa wakiishi nje ya Malindi isipokuwa idadi ndogo sana waliokuwa wakifanya kazi ofisi za serekali au kwenginepo.
Sherehe nyingi hasa za harusi huwa ni za mchanganyiko, sherehe hizi hushiriki wakaaji wote wa Malindi hata huzuni, kukihudhuriwa na watu bila ya ubaguzi wowote.
Kwa sababu nimeweza kuhudhuria sherehe nyingi naweza kuzieleza tarabitu zote, zilioko katika baadhi ya ngoma ambazo nilioshiriki au kuona kama vile Gwaride Shabuwani na sherehe ya Maulidi. Hapa chini mimi nitaeleza kwa kadri ya uwezo wa kukumbuka hizi ngoma za kitamaduni ambazo mimi ninazi fahamu au nilishiriki

NGOMA ZA KITAMADUNI –MALINDI
Hapa nitajaribu kuzieleza ngoma hizi za kitamaduni kwa uwezo wa ujuzi wangu na vile ninavyo zifahamu. Ngoma zenyewe ni kama zifuatavyo 1. Gwaride 2. Shabuwani 3. Kirumbizi 4. Goma  5. Vugo 6. Lemama 7. Mwaribe 8 Gonda na 9. Sherehe za Maulidi 

     1.      GWARIDE
Gwaride Malindi kulikuwa na vikundi viwili kimoja kikiitwa Kingi na cha pili kilitwa Sultan. Kikundi cha Kingi kilikuweko upande wa Kwajiwa kuelekea barani na kikundi cha Sultani kilikuweko Shella.
Hata hivyo vikundi vyote vilikuwa, vimekusanya wafuasi kutoka Kwajiwa, Shella Bomani na Barani. Kuna wafuasi pia walotoka Ganda, Mkaomoto, Mgurureni, Mere na Kakuyuni wafuasi walikuwa ni wa mchanganyiko wa makabila
     a)      Viongozi wa kikundi cha Kingi walikuwa kama wafuatao
i.                    Marehemu Uba – (Abdurahaman A. Chocha – kama captain
ii.                  Mzee Musa marehemu
iii.                Marehemu mzee Khamisi Dobi – mpigaji gwaride.
iv.                 Marehemu – Mwakatwa mpigaji tarumbeta
v.                   Marehemu Pekele – mpiga kigoma

     b)      Viongozi wa kikundi cha Sultan
i.                    Marehemu Bakari Ali
Marehemu mzee Ali Shiheli – pia mfadhili
ii.                  Mzee Omar Shee   mpigaji Tarumbeta
Marehemu Duru mpiga tarumbeta
iii.                Mpigaji gwaride marehemu Mbaruku / drama
iv.                 Mpigaji gwaaride marehemu Azizi Breki

c)   Kwa kawaida Gwaride lilikuwa na vikosi vifuatavyo
i.                    Kikosi cha wazee kikogozwa na captain
ii.                  Kikosi cha Arab Scouts
iii.                Kikosi cha Navy na Askari wengine.
iv.                 Kikosi cha Cowboy

  d)     Mimi nilikuwa ni mfuasi wa Kingi na nilicheza katika kikosi cha Arab scout, wakati huo nilikuwa na              umri kama 12 and 13 hivi.
          i.      Arab Scout walikuwa wakivaa vazi la suruali nyeupe na shirt jeupe na kichwani kuvaa  igal – igal ni kitambaa unachovaa kichwani na huzuiliwa na mfano wa kamba nyeusi uliosukwa vizuri sana – igalinatoka Arabuni na sana ni zawadi wanaokwenda Makka kuhiji huleta kama zawadi. Mchezo wa kikosi cha Arab Scout ni mchezo ulio makini wenye utulivu na kuchezwa kufuatia mlio na mdundo wa ngoma.

        ii.    Kikosi cha wazee huwa kina ongozwa na captain ambae anakuwa mbele. Wazee huwa wamevaa rasmi nguo tafauti tafauti za kupendeza. Wengine huwa wamevaa suti natai, wengine suruali na shati na dhalika wote ukiwangalia wako maridadi kwa mapambo ya namna namna.

 iii.     Kikosi cha navy huvaa mavasi ya navy kiongozi akivaa mavazi ya Officer wa navy wa wanao fuata,                huvalia nguo za askari  wa Navy (ukiona utafikiri ni navy wa kweli)  na kuna wale wanavaa Mavasi au          nguo za askari wengine.
   
iv.      Pia ni mchezo wa makini wenye haiba ya kipekee na mara nyinge huenda march kama askari wa kweli.

 v.     Kikosi cha cowboy –kikosi hichi watu wana valia kama cowboy katika picha za Kiamerika, kiononi 
      ametia pastola ya bandia na kamba ya kufungia ngombe ame funga kiunoni – kama vile Waamerika               wanaochunga ngombe huvaa na kuonekana katika film za cowboy za Kiamerika.



         Pia huwa wamevaa viatu venye visigino vya juu vikifunguwa hadi juu ya macho ya miguu. Kuchezwa   kwake nikwa vishindo na machachari, wakirusha kamba na kupiga firimbi. Mchezo wa cowboy haukuwa ukichezwa kwa makini kabisa, ulikuwa na harahati nyingi za kimazoezi kama mchezo wa P.E shuleni. Mchezo wake ulikuwa ukifurahisha sana mara nyingi wao hawafuati mtindo wa ngoma inopigwa bali walikuwa na miondoko yao wenyewe wakifuata kiongozi wao anavyo fanya.

        e) Kawaida upande wa Kingi walikuwa kuanzia Captain 1) Wazee 2) Navy, 3)Arab scout and 4)                  kumalizikia Cowboy.  Wapigaji ngoma na tarumbeta wali kuwa mwisho wa vikosi vyote.

      f) Kingi walikuwa wakianzia ngoma upande wa “Baipasi” sasa round about “ kufuatia njia hii kuja chini hadi kwa hoteli ya Manos na Said Kafiri (wakati huo hapakuwa na majengo ya hivi sasa kama Wananchi Bar, Lamu Hotel, Tana Hotel na Habib Bank, mjengo mengi ni mapya.
        Ngoma huanzia saa kumi na moja na nusu au kumi na mbili hadi ififikia karibu na Wananchi Bar, huwa ni     takriban saa moja usiku. Kipande cha Wananchi Bar mpaka Habib Bank kuanzia saa moja jioni hadi saa tatu unusu usiku. Hii huwa ni kapande cha kuchezwa ngoma ya Mserego kwa makini na utulivu sana. Kila mchezaji alikuwa akicheza kwa madaha na kuonyesha ubora na uhodari wake wakucheza. Huu ndio wakati watu wana kuja kuangalia wakiwa ni wengi sana. Wengine huwa wana watazama marafiki zao, au wazazi kuwatuza watoto wao wanao chezo. Wengine wali kuwa – wakizawadiwa mashada ya kila aina ya usimini, viluwa, makoja ya karatasi – tuseme kila ina ya mapambo huwa wakipambwa wachezaji, hata pesa.

        g) Tukiangalia upande wa Sultan ni dhamu yake hufanana sana na Kingi. Wao huwa wakianzia bara bara ya kutokea kwa Bakshweni yaani Malindi Cylce Mart wakushukia chini kupitia kitanguni kwa Masoud kuja Kitaru cha Naran na kupita kwa Abdalla ngozi (sasa Dosajee) kuja kwa Bawali haluwa mpaka msikitiwa Bohora. Nidhamu za kucheza ni zile zile kama za kingi bali kula kikosi na kikundi kinaonyesha uhodari na ujuzi wake kuweza kuvutia watu wengi kuja kuwaangalia

        h) Gwaride huchezwa kwa musimu yaani katika miezi mitatu ya Kiangazi na ilikuwa ikichezwa kila siku ya ijumaa pili jioni – kuanzia saa kumi na moja na nusu hadi saa tatu na nusu usiku.
        Kingi humaliza dori lake kwa marehemu mzee Swaleh Chocha –baada kutoka kwa marehemu mzee          Uba kupiga saluti wana kuja kwa marehemu mzee Swaleh kupiga saluti na kuvunja ngoma
      Upande wa Sultani vile vile ili kuwa ikipitia kwa marehemu mzee Shikeli na marehemu Bakari Ali na kumalizikia katika uwanja wa marehemu Abdalla Swaleh –Mkwajuni

         i) Katika Gwaride kuna mambo ya ziada nyakati za mwisho wa musimu kwani kila kikundi kinataka kipate ushindi wa mwaka ule. Kila kikundi huleta wachezaji wa sarakasi kutoka Mombasa na Tanzania wa kila aina, kama miguu ya miti, wenye hutowa moto midomoni, kuna wenye vituko aina aina. Mimi nitaeleza siku ya mwisho (finali) yani siku moja katika maisha ambayo ilinivutia na kunifanya kuto sahau ni siku hii ya finali.
Kwa upande wa Kingi wao waliunda meli kubwa sana iliwekwa juu ya lori, meli hii iliundwa kama manuwari ya kweli ambayo ilikuwa na askari wa kawaida wa navy pamoja na maofisa ikienda taratibu juu ya lile roli – katika udogo wangu mimi nilidhania ni kweli manawari ya kweli na wale askari wa ‘navy’ ni wa kweli.(manwari ni meli ya kivita ya navy).

Yule captain alisimama ma kwenye Manwari (meli ya Navy) na mkewe amevalia veli na taji kama malkia. Huku wakipungia mkono watu, niilifikiri ni mfalme na malkia kweli vile walivyokuwa wamevaa, kweli ilikuwa jambo la kupendeza na la ajabu sana.
Manwari ilikua imekuja saa za mwisho baada ya saa mbili usiku lakini kabla ya hio manwari, kulikuwa na mtu aliekuwa akitembea juu ya kamba akicheza na moto.
Zamani Malindi kulikuwa na minazi mingi ubavuni pa hoteli ya Manoos palikuwa na mnazi na nyuma jumba hili sasa la Lamu Hotel kulikuwa na mnazi mwengine, takriban masafa ya futi 150 au 200. Kamba ilifungwa kutoka mnazi uliokuweko kwa Manoos hadi katika manzi uliokuwako juma ya Lamu hotel.

Yule mchezaji alipanda mnazi ulikuwako nyuma ya Lamu Hotel ambao ulikuwa haunekani na watu. Tulishutukia tunaona mtu akitembea juu ya kamba huku akirusha moto huku na huku mara ingine alitowa moto mdomoni. Watu wote wakasahau gwaride wakashughulika kuangalia sarakasi hii. Alio kuwa akiyafanya ni mambo ya ajabu sana. Mara nyingine kujifanya kama anataka kuanguka, kisha akarudi kama alivyo kuwa, watu wakaona mambo ya ajabu ambayo sote hatujapata kuona.
Nilielezwa kuwa Yule mchezaji wa kamba ameletwa kutoka Tanganyika (Tanzania) na wengi walikuwa ni hisia kuwa moto ulikuwa ukitoka mdomoni ni kweli bali ni  kwa ajili ya mafuta aliokuwa akitaia mdomoni na kuvuzia huku ameshika moto mbele ya mdomo akaonekana kama unatoka mdomoni.

J) Kwa upande wa Sultani walikuwa na vioja vyao pia. Walileta watu wa maguu ya miti wakiteza kila na  namna wakirusha vitu na kunyaka na kutowa moto midomoni.
Onyesho kubwa la ajabu ilikuwa kuba kubwa liloundewa kwenye lori. Katika kuba kulikuwa na  watu walicheza kama nachi za kihindi za kupendeza na kuvutia sana kwa vile watu wengi wa Malindi nyakati hizo walikipenda sinema za Kihindi.
Maonyesho haya ya kiajabu huja saa za mwisho ikiwa kila kikundi kikivutia kwake. Hizi ndio sherehe za mwisho zenye kuonyesha upeo wa uhodari wakucheza wakishindana  kupata jamhuri kubwa ili kupta ushindi wa mwaka ule.

k) Kawaida Gwaride huanzia saa kumi na mbili jioni kilile cha mchezo ni kutoka saa mbili usiku hadi saa nne kuanzia saa nne huwa zinapandia mitaani Kingi ina elekea Kwajiwa na Sultani huelekea Shella ikifika saa nne unusu usiku huwa ngoma zamesha vunjwa na kila  mtu ameenda kwake.

Nyimbo mashahuri sana zilikuwa zikiimbwa na zinao hamasisha wachezaji wa gwaride kwa mfano.
Endao pwani na Nende
Nenda kwamwambie
Kenya basi haina ahadi
Haiati mzishiwe
Chicha na kanada
Shauri yao.

Ya pili – Nyumbu eeeerero nyumbu rero
Watetea mwana siwako
Nyamaza Kingi kulia.

     2.      SHABWANI
     a)      Hii ni ngoma ya Kiarabu, hasa kutoka jamii ya Kihadharami. Ilifika hapa Malindi na Mombasa karne nyingi ziliopita na kutezwa katika sherehe nyingi kama za harusi na za Maulidi wakati wa zefe. Shabwani ni ngoma ambayo inachezwa kwa harakati za kuruka ruka na mikononi wenye kucheza  huwana bakora au fimbo wakati wakicheza zile fimbo huwa zikirushwa rushwa juu na huku wakiiimba. Arabuni waliokuwa wanao cheza huwa wana tumia panga lakini hapa watu hutumia fimbo au bakora.
     b)      Ngoma ya shabwani hutumia ngoma moja au mbili, matasa na vigoma. Ngoma ya tasa ni huambwa kwa ngozi.(yaani karai liloombwa kwa ngozi) 

     c)      Hii goma ya tasa ni lazima iwe itakanzwa moto wakati wa kutumika na kupigwa kwa vijiti viwii vipana virefu. Kupata mlio mzuri ni lazima vile vijiti viwe vigumu na tasa limeoka moto uzuri.

     d)    Kuanza kucheza shabwani – wachezaji hujipanga laini mbili za kulekeana yaani kuangalian uso kwa uso. Wakati huo wenye kupiga tasa huwa wanazikanza moto.

     e)   Kiongozi huingia katikatii na kuanza kutowa shairi la fumbo na kulekea laini moja. Na wale wachezaji waliolekewa waitika kama vile kiongozi anavyo imba. Wakisha itikia anazungukia laini ya pili kutowa shairi ya jawabu yahilo fumbo. Sasa wachezaji wakaanza kuimba na kujibanza wakati huu wenye ngoma wataanza kupiga na shabwani kuanza ana wachezaji wote wakielekea upande moja wakiruka ruka na kurusha fimbo / bakora walizo nazo mikononi mwao kwa nidhamu ya kufuatia mdundo wa ngoma.

     f) Shabwani – watu waenda wakicheza, wakifika mita 150 au 200 mita, hubidi wenye kucheza waanze upya, kwani tasa huwa limeanza kupoa na mlio huwa si mzuri. Shabwani itaanzwa kama vile ilivyoanza mwanzo.

     g)    Shabwani zilikuwa ni tatu, kutoka Mombasa Malindi na Mambrui. Shabwani hizi mara nyingi hushindana wakati wa sherehe za Maulidi.Mamburii na Malindi Shabwani ya Malindi na Mambarui walikuwa wakishindana wakati wa sherehe za Maulidi ya Kipini.
     h)      Shabwani ilikuwa ikichezwa sana katika sherehe za harusi wakati wa kutia hina na kumnyowa bwana harusi na kumpeleka nyumbani.

     i)     Shabwaini huchezwa siku ya kutiwa hina Bwana harusi. Sherehe kufanyika usiku wa siku ya kuingia ndani, siku ya kuamkia nikaka. Sherehe hii hufanywa katika uwanja karibu na nyumba ya bwana harusi nayo inaanza baada ya ishaa na kuendelea hadi saa nne usiku au zaidi.

     j)     Katika sherehe ya kunyolewa  bwana harusi ambayo hufanyika katika mmoja ya kitanguni(bustani ya miti ya matunda na maua) Malindi kulikuwa na vitangi vitatu, kitanguini kwa marehemu Maalim Balala, kitanguni kwa kina Marehemu Masudi (sasa kuna star Hospitali) na kitanguni cha Barani (sasa kuna gareji ya marehemu Mohamed Mzuengu nyuma ya duka ya la Sheikh Salim).
Sherehe ya kunyolewa, bwana harusi akiwa ananyolewa shabuwani wakati huo huwa inachezwa. Akisha kunyolewa huchukuliwa Yule bwana harusi na shabwani hadi pale atakapo funga, Nikaha.  Akisha funga Nikaha baada ya ishaa, bwana harusi hupelekwa kwa mkewe kutowa mkono na kisha kupelekwa kwake nyumbani.
     k)      Shabwani ya Malind ilikuwa ikisimamiwa na
     (a)   Marehemu Swalehe Chocha,
     (b)   Marehemu Salim Bazmale
Shabwani ya Mambrui ikisimamiwa na:-
(a)Marehemu Omar Alwan
(b)Marehemu Mzee Nassor
    
   3.      KIRUMBIZI
     a)     Kirumbizi huchezwa sana na Wabajuni na Waswahili lakini huchezwa katika sherehe zote za harusi hata ya Kiarabu. Kirumbizi Kawaida huchezwa na wanaume pekee, watu hufanya duwara kubwa wa chezaji na wano piga ngoma huwa ndani ya hilo duwara au boma. Kirumbizi, ni mcheza wa bakora ua fimbo Watu wa kucheza kirumbizi katika harusi. Wanawake huwa kwenye jukwaa lilositiriwa na uwa wa makuti. Wale wanawake huwa wanawaona wanaocheza kirumbizi lakini wachezao na wanaume wengine hawaoni wale wanawake. Wale wanawake husherekea nakushangilia kwa kupiga vugo na kwa nyimbo.

     b)      Kawaida ya kirumbizi inategemea Yule mwenye kuitayarisha, kuna wanao cheza kwa siku moja, siku tatu au siku saba. HIvi inatagemea mfuko wa Yule mwenye kutayarisha au mwenye kuweka kirumbizi na kuandaa.
     c)       Siku ya mwisho ya kirumbizi, ni siku ambayo Bwana harusi huja uwanjani na yeye kushiriki.Hapo huwa ndio kilele cha sherehe hio. Bwana harusi – yeye huwa amepambwa kwa mashada, viluwa na makoja. Yeye huinuliwa na baba mkwe na kucheza nae. Kucheza kwao huwa ni kwa taratibu na heshima pamoja na taadhima kubwa. Huko wanawake wakishangilia zaidi ya siku zilio pita.
Wakati bwana harusi akicheza watu hugaiwia maji ya sharebati na tambuu. Tambuu hizi ni tafauti kwa vile huwa zina pambwa kwa karafuu.

     d)      Uchezaji wa kirumbizi huchezwa kwa watu kutumia fimbo au Bakora, mchezaji huchukuwa fimbo au bakora na kuingia uwanjani na kumrushia fimbo au bakora Yule atakae cheza nae.
     e)     Wakiisha ingia kiwanjani huwa wanacheza kwa upole n atarabibu kwa kufuatao mdundo wa ngoma. Wachezaji huzunguka wakicheza kwa mfano wa koo la tausi au bata mzinga anapo mtaka tausi au bata mzinga jike. Huzunguka wakicheza kwa haiba na utaribu wenye kupendeza sana. Ngoma ikitangwanya na kulia kwa sauti kubwa, sasa wachezaji kurushiana fimbo au bakora moja moja. Wala hakuna kurushiana kwa nguvu za kupita kiasa bali kwa nguvu ya wastani kwa haiba na madaha.
Yule aliorushiwa bakora au fimbo mara ya kwanza ataichukuwa fimbo au bakora ya mwenzie amrushie mwengine na hivi mchezo uanandelea. 
     f)       Ngoma zinao tumika ni ngoma za kawaida na msondo, tasa, zumari au tarumbeta. 

4. GOMA 


     Goma hii huchezwa sana na Wabajuni. Ngoma yenyewe ni ngoma ambayo huchezwa bila vishindo wala harakati nyingi. Ni ngoma inayochezwa kwa ustarabu na haiba ya juu.
     Wachezaji hucheza kwa makini wakifuatia mdundo wa ngoma. Huechezwa kwa makini sana ya hali ya juu ya utilivu kutaka kuona harakati zao za kucheza ni lazima uwe na makini kutizama ndio utaona harakati za kucheza.
    Wachezaji huwa wamevaa kanzu nyeupe na kofia za vito, bakora mkono wa kulia. Bakora huwa imewekwa begani na huwa inainuliwa mara moja moja kufuatana na mdundo wa ngoma. Wachezaji huwa wamepambwa kwa mashahada ya maua na pengine kosaja la pesa.
     Wapigaji ngoma huwa wanaelekea wale wachezaji. Ngoma zenyewe ni zile za kawaida kama a kirumbizi, tasa na zumari.  Goma inaweza kuchezwa kwa muda mrefu na huku watu wengine wakiimba nyimbo tafauti tafauti.

     5.      VUGO
Hii ni ngoma inayochezwa na wanawake wa Kibajuni na Wakiswahili. Ngoma yenye hutumika katika sherehe nyingi kama nilivyo eleza hapa nyuma katika kirumbizi na kupeleka bi harusi na shrehe nyinginezo.
Ngoma huchezwa na wanawake, wakiwa wameshika pembe na kigongo kidogo cha kumpigia pembe. Pembe hupigwa kufuata mlio wa ngoma na mara moja moja huuinuliwa juu kichwani zikipigwa kwa nguvu huku wakiemba mashairi mengi mazuri
Ngoma hii huchezwa na mchanganyiko wa wanawake lakini zaidi ni Wabajuni na Waswahili.

      6.      LELEMAMA
Hii pia ni ngoma ambayo Huchezwa na Wabajuni, Waswahili na wazaliwa wa Kiarabu. Ngoma hii sana huchezwa siku za harusi. Pia hii inategemea wezo wa mtu anae cheza au anaendaa harusi, yaani kucheza kwa siku moja au tatu au zaidi lakini hazipitishi saba.
Ngoma yenyewe huchezwa na wanawake wanao vaa kanga peikee. Kanga ndio nguo rasmi ya kucheza lelemama, kawaida lelemama huchezwa ndani ya uwa yaani boma liljengwe kwa makuti wanaohudhuria ni wanawake pengine isopokuwa wale wapigaji ngoma huwa waume.
Lelemama huchezwa na wanawake wakiwa juu ya mabao wakiwa wamevalia leso zao (kanga) zilio safi na mara nyingi huvaa sare, wachezaji huwa wamejipamba kwa vilua, mashada ya asmini yalio fungwa vichwani. Kila mchezaji huwa ana vigongo viwii ambavyo urefu ni kama inchi 6.

Lemamama huchezwa kwa makini na kuyumba yumba kulia na kushoto kwa kufuata mlio wa ngoma, lelemama pia huchezwa kwa makini na utulivu wa hali ya juu. Wanawake wengine huwa wamekaa chini kwenye majamvi wakipiga makofi na kuimba. Kufuata sauti ya zumari au tarumbeta.
Kulikuwa na vikundi viwili vya lelemama cha kwanza Karisosa na cha pili ni Sultani Karisosa hilikuwa ni kikundi ambayo kime jihusisha na wafuasi wa gwaride la Kingi na Sultani wamejihusisha na kundi cha Sultan. Mara nyingi walikuwa wakishindana.

     7.      MWARIBE
Mwaribe haswa ni ngoma ya Kiswahili lakini huchezwa na makabila kadhaa. Kawaida huchezwa na wanaume na wanawake. Waume wakiwa upande mmoja na wake wakiwa upande mwingine wakiwa wameangaliana uso kwa uso.
Ngoma zinaotumika ni za kwaida lakini hutumika na msondo (msondo ni ngoma ndefu) mwenye kupiga huwa amesimama na ngoma ameitia katikati ya miguu ikizuiliwa na magoti mawili. Pia hutumika na zumari.
Ngoma ikianza kuchezwa na watu hucheza na kuimba mwanmke huja katikati akicheza kwa muda kisha akaenda upande wa wanaume akamtowa mwanamume kucheza nae, watacheza pamoja kwa muda pale katikati. Kiasha yule mume wa atamtowa mwamke mwengine naye watacheza pamoja kwa muda pale kati kisha yule mke atamutowa mwamume mwingine na wataendelea kucheza yule mwanamke wa kwanza atatoka katikati ya uwanja. Mwanamke wa pili atacheza kwa muda wa baadae kumtowa mwanamume mwengine msitari wa waume na ngoma kunaendelea. Ngoma itaeendelea hivi hadi kuvunjika.

     8.      GONDA
Gonda ni ngoma ya Kimijikenda ambayo huchezwa sana na Wagiriama. Ngoma hii kuchezwa kwa utulivu sana na ngoma yeyenye kuchezwa kwa mdundo mzuri hasa kwa wanaume. Wanaume wanaocheza Gonda huvaa shuka ndefu yenye maridadi ya matavuo chini ukingoni. Kifua huwa wazi lakini huwa kimepitishwa na ukanda wa nguo iliofungwa kwa umeridadi kutoka bega hili kushuka katikati ya mwili hushukia kiunoni upande mwengine yaani hutoka bega la kulia ikishuka upande wa kiuno wa kushotoni, nguo zenyewe huwa zinatiwa maridadi mazuri. Pia ukanda mpana ambao hufungwa kiunoni namna ya pekee. Kichwani wanavaa kofia za tarbushi nyekundu.

Ngoma hii huchezwa sana na wazee ambao hucheza kwa madaha na Makini huku wakirusha migwisho na kupiga firimbi gonda ni ngoma yenye haiba sana na huchezwa sana na wazee katika sherehe maalumu.
Wanawake kama kawaida huwa wamevaa mahando yalio malkubwa, huku wakicheza na kuimba na kupiga vigelegele.

Waume hucheza na wanawake wakiimba, huku waume wakicheza miguuni   huwa wamefunga njuga na mikononi wamevaa meridadi ya ngozi. Wakicheza hutetemesha mikono na kupiga miguu yao chini ili zile njuga  zipate kulia.
Ngoma zake ni za kawaida na msondo na kupiga debe kwa vifimbo pia huvuvia pembe na kupiga zumari Ngoma hii huchezwa hadi wenyewe kuchoka. Gonda ni ngoma ninaopenda nawe utapenda kuangalia sana.

     9.      MAULIDI
Maulidi singoma bali ni sherehe ya Kiisilamu ya kukumbukwa kuzaliwa kwa mtume Mohamed (S.A.W) Maulidi huwa yanasomwa wala hayachezwi.
Kuna misikiti mengine husoma maulidi kila siku ya alkhamisi baada ya swala ya magharibi. Pia husoma katika sherehe za Nikaha yaani harusi au mtu akipenda kusoma maulidi.
Maulidi inatoka katika neno la Kiarabu “Maaulid” kuzaliwa yaani “Birthday” 
Sherehe kubwa ya maulid husomwa mara moja kwa mwaka katika mwezi wa mfugo sita Kiswahili “Rabi – Awal” karibu, sherehe hii ya maulidi husoma katika miji kadhaa kama vile Lamu, Mambrui, Kipini, Malindi, Mombasa na Nairobi, na kwenginepo 
Siku ya maulidi katika miji huanzwa kwa sherehe za Dhefe, dhefe ni sherehe moja huchezwa na watoto na wazee kila madrasa ambyo inayoshriki ina dhefe yake. Kila dhefe, inakasida maalumu wanazo ziimba za kusifu mtume Mohammad (S.A.W)
Kuna kwasida za Kiswahili, kiarabu na siku hizi za kimijikenda.

Dhefe huanza baada ya Al-asri. Maulidi huanzia msikiti wa Jumaa na kuandamana kupitia baharini dhefe husimama katika Msikiti wa Shella wakaombea wafu dua. Wakitoka hapo wanakwenda msikiti wa Biniamuni-sasa “Masjid Qubaa” hapa pia husimama wa kuombea wafu dua katika maziara hapo kwa msikiti kwa Biniamuni:
Kutoka hapo dhefe ambazo zina fika karibu ishirini hutoka madrasa tafauti tafauti kama vile kutoka madrasa za Malindi, Mambrui Kakunyeini, Takaungu na kwenginepo. Kila madrasa huwa zina imba qasida tafauti na kwenda mrama huku wakitafautiana  huku wakipiga matwari na vigoma . Maulidi haina tarumbeta au zumari.  Qasida husomwa kwa mahadhi mazuri ya kuvutia .

Katika maulidi makubwa ya Malindi Mambrui, na Kipini mara nyingi kupatikana Ngoma ya shabuwani, wakati wa zamani huwa na mashindano ya shabuwani baina ya Malindi, Mombasa na Mamburui. Mashindano haya hufanywa siku ya Maulidi makubwa ya kila mwaka.




PREPARED BY
ABUD SALIM MBARAK BAZMALEH
WINNER OF SPECIAL CATEGORY, HUMAN RIGHTS AWARD, 2006 
+254 -724338113



SUBMITTED TO DORIS KAMUYE
MALINDI MUSEUM – WEBB MEMORIAL LIBRARY